Rais wa Senegal Macky Sall amerejesha wadhifa wa Waziri Mkuu nchini mwake miezi miwili baada ya uchaguzi wa bunge uliokuwa na mivutano.

Rais wa Senegal amemteua aliyekuwa waziri wa uchumi Amadou Ba katika wadhfa huo mpya ambaye pia ataliongoza baraza la mawaziri.

Amadou Ba, mtaalamu wa masuala ya kodi mwenye umri wa miaka 61 amewahi pia kuwa waziri wa mambo ya nje wa Senegal.

Uteuzi wa Ba ambao umeifufua tena nafasi ya waziri mkuu katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi umefanywa baada ya wadhifa huo kuondolewa mnamo mwezi Aprili mwaka 2019.

Amadou Ba amesema kwenye televisheni ya taifa kwamba vipaumbele vikuu ambavyo rais Macky Sal ameviainisha ni pamoja na kuboresha hali ya uchumi kwa wananchi wa Senegal, kudhibiti mfumuko wa bei, usalama, makazi bora, mafunzo ya ufundi stadi, ajira na shughuli za ujasiriamali.

Uchaguzi wa Bunge nchini Senegal ambapo muungano wa Rais Macky Sal ulipoteza wingi wa viti bungeni.

Nafasi hiyo ya Waziri Mkuu imeanzishwa wakati Senegal inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, ambayo kwa sehemu kubwa yanatokana na janga la COVID-19 na athari zinazoukumba ulimwengu kutokana na vita vya nchini Ukraine.

Wasiwasi juu ya utawala wa Rais Macky Sal unaendelea kujitokeza huku akituhumiwa kwa kutaka kuvunja ukomo wa mihula miwili uongozini hatua itakayomwezesha kugombea urais tena ifikapo mwaka 2024. 

Maandamano makubwa yalifanyika nchini Senegal mwaka jana wakati Ousmane Sonko, mpinzani mkuu wa Sall aliyeibuka wa tatu kwenye uchaguzi wa rais mwaka 2019 alipokamatwa kwa tuhuma za ubakaji ambapo amekanusha kuhusika.

Rais Macky Sall pia ametofautiana na mshirika muhimu kwenye kambi yake, waziri mkuu wa zamani Aminata Mimi Toure, ambaye hakuchaguliwa kuliongoza bunge la kitaifa na tangu wakati huo ameulaani utawala wa Sal kwa “ukosefu wa haki.”

Rais Samia ashiriki mazishi ya Malkia Elizabeth II
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 18, 2022