Rais wa Sri Lanka, Maithripala Sirisena amefanya mabadiliko katika vikosi vya usalama kwa kushindwa kuchukua hatua licha ya kupokea taarifa za onyo la mashambulizi ya kipindi cha Pasaka yaliyosababisha vifo zaidi ya watu 350.
Amefanya uamuzi huo baada ya maafisa kushindwa kuchukua hatua licha ya kupokea taarifa za onyo la uwezekano wa kutokea mashambulizi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 350 wakati wa kipindi cha Pasaka.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba maafisa wa upelelzi wa Sri Lanka walionywa na India saa kadhaa kabla ya kutokea mashambulio hayo, lakini haijulikani wazi iwapo maafisa hao walichukua hatua yoyote kufuatia onyo hilo.
Aidha, katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni kwa taifa, Rais Sirisena amesema kuwa atambadilisha mkuu wa vikosi vya majeshi katika kipindi cha masaa 24, na Jumatano aliwataka katibu wa ulinzi na mkuu wa jeshi la polisi kujiuzulu.
Rais Sirisena hakutaja kuwa ni nani atachukua nafasi zao, lakini amesema kuwa alifichwa taarifa hizo za uwezekano wa kutokea mashambulizi na ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya maafisa wote walioshindwa kumuarifu mapema.
Hata hivyo, Polisi wa Sri Lanka wamesema kuwa wamewakamata watu wengine 18 wanaowashuku kuhusika na mashambulizi hayo ya Jumapili ya Pasaka, huku idadi ya vifo ikiwa imeongezeka na kufika watu 359, ambapo kundi linalojiita Dola la Kiislam IS limekiri kuhusika, baada ya maafisa wa Sri Lanka kusema waliojitoa muhanga kwa kujilipua walilipiza kisasi cha mashambulizi ya misikiti miwili ya nchini New Zealand ya mwezi Machi yaliyosababisha vifo 50.