Rais wa Tunisia, Beji Caid Essebsi amelazwa hospitali baada ya kukumbwa na tatizo la dharura la kiafya.
Taarifa hizo zinaifanya nchi hiyo kuwa katika hali ya sintofahamu muda mfupi baada ya kukumbwa na milipuko miwili ya mabomu ya kujitoa mhanga katika mji mkuu wa Tunis.
Essebsi mwenye umri wa miaka 92 anasemekana kuwa katika hali mahututi lakini hali hiyo imedhibitiwa na kuwa anafanyiwa vipimo muhimu.
Aidha, taarifa hiyo imetolewa baada ya madai kusambaa kuwa Essebsi, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2014, amefariki dunia.
Hata hivyo, kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS limedai kuhusika na milipuko hiyo ya mabomu, na kufufua hofu kuhusu utulivu wa taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Tunisia inaonekana kama mfano nadra wa Kidemokrasia baada ya wimbi la mageuzi ya umma katika ulimwengu wa kiarabu mwaka wa 2011 lakini imekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya IS.