Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ametoa wito hii leo wa mazungumzo ya kina ya amani na Moscow, akisema ndiyo nafasi pekee ya Urusi kupunguza uharibifu uliotokana na makosa yake baada ya kufanya uvamizi.
Zelenskiy amesema Ukraine imekuwa ikitoa suluhisho kila wakati la amani na kutaka mazungumzo yenye maana juu ya usalama bila kuchelewa.
Kwa mujibu wa Rais Zelenskiy vikosi vya Urusi vinazuia kwa makusudi usambazaji wa misaada ya kiutu katika miji iliyoko chini ya mashambulizi.
Rais huyo amesema hadi sasa hakuna taarifa za watu wangapi wamefariki baada ya jumba la maonyesho kushambuliwa mjini Mariupol. Wakati huo huo vikosi vya Urusi vimezidisha mashambulizi katika miji ya Ukraine ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kyiv na kituo cha ukarabati wa ndege nje kidogo ya mji wa Lviv, karibu na mpaka na Poland.
Mjumbe wa Urusi katika mazungumzo na Ukraine ya kusaka suluhu ya vita inayoendelea Vladimir Medinsky amesema pande hizo mbili ziko karibu kuafikiana katika mambo muhimu juu ya uwezekano wa Ukraine kutoegemea upande wowote na uanachama katika jumuiya ya kujihami NATO, lakini bado kuna baadhi ya masuala hayajatatuliwa kabla ya marais wa nchi hizo mbili kukutana.