Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amewakosowa vikali viongozi wa mataifa ya Magharibi kwa kutokuchukuwa hatua dhidi ya tangazo la Wizara ya Ulinzi ya Urusi kwamba ingelishambulia eneo la viwanda linalomilikiwa na jeshi la Ukraine.
Akizungumza kupitia akaunti yake ya Telegram usiku wa kuamkia leo, Zelensky amesema hadi sasa hajamsikia kiongozi yeyote wa dunia akizungumzia jambo hilo.
Zelensky amesema kuwa uthubutu unaooneshwa na Urusi unathibitisha wazi kwamba vikwazo vilivyowekwa dhidi yake havitoshi.
Katika hotuba yake hiyo, Zelensky ametaka kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kuwashitaki wanaoamuru na kufanya uhalifu unaoendelea nchini mwake.
Itakumbukwa wizara ya ulinzi ya Urusi March 6, 2022 ilitangaza kwamba vikosi vyake vinadhamiria kulishambulia eneo la viwanda vya kijeshi ikidai kwamba lilikuwa ghala la silaha.
Msemaji wa wizara hiyo, Igor Konashenkov, aliwataka wafanyakazi wote kuondoka eneo hilo huku rais Zelensky naye amewataka wafanyakazi hao kutokwenda kazini.