Rais wa Shirikisho la Soka visiwani Zanzibar ‘ZFF’, Suleiman Jabir, amesema anapambana kurejesha heshima ya soka visiwani humo kutoka la ridhaa na kulifanya kuwa la kulipwa.
Amesema kazi kubwa ni kutoa semina na mafunzo ya utawala bora kwa viongozi wa klabu na timu zote za visiwani Zanzibar, Uguja na Pemba.
Akizungumza kisiwani Unguja, Jabir amesema baadhi ya klabu na timu nyingi za Zanzibar hazina Ofisi maalum, sababu inayochangia kukosa wadhamini wa kuziwezesha klabu hizo kujimudu kwa kufanya usajili mzuri na kuleta makocha kutoka nje.
Amesema timu ambazo zimefanikiwa kujiendesha kisasa ni zile zinazomilikiwa na taasisi kama ilivyo kwa KMKM, Mafunzo na JKU, ambazo zimekuwa zinafanya usajili na kuleta wachezaji kutoka mataifa mengine.
“Tunahitaji kurejesha soka la Zanzibar kuwa la ushindani, kwa klabu kupata wadhamini kama ilivyo kwa Bara, hatuwezi kufika huko hadi kuwapo kwa mafunzo ya utawala bora kwa viongozi, kwa kuziondoa timu kwenye majumba yao na kuwa na Ofisi maalum,” amesema Jabir.