Aliyewahi kuwa Meneja wa muda wa Manchester United, Ralf Rangnick amemtaka Julian Nagelsmann kukubali ofa ya kwenda kuinoa Tottenham Hotspur, ambayo kwa sasa inatafuta Meneja mpya baada ya kumfuta kazi Antonio Conte.
Rangnick, ambaye aliwahi kufanya kazi na Nagelsmann kwenye klabu ya RB Leipzig, amemtaka bosi huyo wa zamani wa FC Bayern Munich kukubali kazi ya kwenda kuinoa Spurs kwa sababu ni timu yenye miondombinu sahihi katika soka.
Akizungumza na Sky Sports Deutschland Rangnick amesema: “Tottenham ni timu inayovutia kwenye namna nyingi sana. Wana uwanja mzuri sana duniani. Wana miundombinu mizuri ya kufanya mazoezi na wanaye Daniel Levy ambaye amekuwa kwenye klabu hiyo kwa miaka mingi.”
“Kama Tottenham waanamuhitaji kweli Julian Nagelsmann, basi litakuwa jambo jema kwa timu hiyo kuajiri pia mkurugenzi wa michezo ili kumsaidia. Spurs si timu inayotarajia mafanikio ya haraka. Hivyo, ni mahali panapovutia kwenda kufanya kazi.”
Spurs hivi karibuni ilimfuta kazi pia aliyekuwa Meneja wa mpito Cristian Stellini baada ya kukumbana na kichapo cha mabao 6-1 kutoka kwa Newcastle United, huku wakiruhusu nyavu zao kuguswa mara tano ndani ya dakika 21.