Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amekabidhiwa kijiti cha uongozi wa Umoja wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka kwa rais wa Misri Abdel Fattah al Sis, katika mkutano wa Umoja huo huko Addis Ababa nchini Ethiopia.
Akizungumza mbele ya viongozi wa Umoja wa Afrika, mawaziri, wanadiplomasia, rais wa Misri Abdel Fattah al Sis, amesema ilikuwa ni fahari kubwa kwake kuwa kiongozi wa Umoja wa Afrika kwa kipindi cha mwaka mmoja, Amesisitiza kwamba yupo tayari kuandaa mkutano wa kilele wa kusaidia kuunda jeshi la Afrika kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Cyril Ramaphosa amethibitisha kwamba ataitisha mkutano usiokuwa wa kawaida wa wakuu viongozi wa Umoja huo jijini Pretoria mwezi Mei kuzungumzia maswala ya usalama, mkutano ambao kauli mbiu yake itakuwa ni kukomesha mapigano.
Wazungumzaji wote katika kukao hicho wamegusia pia swala la Palestina na kubaini uungwaji wao mkono kwa madai ya Wapalestina. Katika hatua nyingine Cyril Ramaphosa pia alisema kwamba anaunga mkono haki ya kujitawala kwa watu wa Sahara Magharibi.