Mshambuliaji kutoka nchini Brazil na Klabu ya Barcelona, Raphael Dias Belloli, ‘Raphinha’, amesema kikosi chao kinapaswa kuendelea kuonyesha kiwango kizuri katika michezo ijayo zijazo ili kujihakikishia nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), msimu huu 2022/23.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Leeds United ya England ametoa kauli hiyo baada ya kikosi cha FC Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Real Betis katika Uwanja wa Spotify Camp Nou, Hispania juzi Jumamosi (Aprili 29).
Katika mchezo huo, mabao ya FC Barcelona yaliwekwa kimiani na Andreas Christensen, Robert Lewandowski, Raphinha na Guido Rodríguez aliyejifunga.
Raphinha amesema ili kikosi chao kitwae ubingwa wa La Liga msimu huu, kinapaswa kuendelea kuonyesha kiwango kama kilichoonyesha katika mchezo huo uliopigwa juzi.
“Xavi alituonya, tulijua tulihitaji kuwa bora tukiwa na mpira. Kama tunataka kushinda ligi, tunapaswa kucheza kama hivi,” amesema.
Amesema hawapaswi kurudia makosa waliyofanya katika mchezo dhidi ya Rayo Vallecano ambao kikosi hicho kilikubali kichapo cha mabao 2-1.
“Mchezo dhidi ya Rayo ulikuwa mgumu. Tulitakiwa kujibu kwa ushindi,” ameongeza kusema.
Hadi sasa FC Barcelona inaongoza msimamo wa La Liga ikiwa na alama 79 katika michezo 32, ikifuatiwa na Real Madrid yenye alama 68 baada ya kushuka dimbani mara 32.