Katika kuhakikisha kuwa mkoa wa Tabora unajiletea maendeleo, Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote mkoani humo kuwashirikisha Wakaguzi wa ndani na Maafisa wa Ugavi na Ununuzi wakati wa ukaguzi miradi mbalimbali katika maeneo yao ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora na inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.
Ameyasema hayo mjini Tabora wakati wakati anafunga mafunzo ya siku tano ya Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri zote ya Mkoa wa Tabora yaliyohusu mbinu mpya za ukaguzi wa hesabu kufuatia mabadiliko katika ukusanyaji wa mapato na maduhuli ya Serikali kuendeshwa kwa njia ya mtandao.
“Nawagiza Wakurugenzi katika Halmashauri zote nane za Tabora kuhakikisha wanaongozana na Wakaguzi wa Ndani na Maafisa wa manunuzi ili waweze kujiridhisha kama miradi inatekelezwa inalinga na fedha iliyotolewa na hakuna udanganyifu wowote uliofanyika” amesema Dkt. Ntara
Hata hivyo, Dkt. Ntara ametoa wito kwa Wakaguzi hao wa Ndani waliopata mafunzo hayo na mbinu hizo za kisasa walizofundishwa kufanya kazi kwa ufanisi na kuzisaidia Halmashauri kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali katika Halmashauri zao katika makusanyo ya maduhuli na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao.