Katika hatua nyingine Rais Samia amesema wananchi wanahitaji mitaji midogo midogo hasa katika uzalishaji wa bidhaa zao ambazo hazina viwango kutokana na kukosa vifungashio vinavyovutia sokoni hivyo TASAF isaidie kuwainua na kuwabadilishia mtazamo.
Pia Rais amewaonywa baadhi ya wafanyakazi walafi kuepuka ulaji wa pesa za mradi huo kwa manufaa yao binafsi kwani fedha hizo zinatokana na mikopo ambayo hulipwa na watanzania wote hivyo wazifanyie kazi iliyokusudiwa.
Awali kabla ya kumkaribisha Rais Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amesema Rais Samia anaendelea kuweka historia kwa kujenga uchumi na amewathibitishia Watanzania jinsi anavyowajali kwa kuwapatia magari yatakayosaidia utekelezaji wa majukumu na kuwahudumia.
Amesema mradi wa huo wa TASAF awamu ya tatu sehemu ya pili utasaidia kuwafikia wahitaji katika vijiji, shehia na kaya zenye wakazi zaidi ya milioni sita na kufanya mpango huu wa maendeleo wa taifa kutekelezwa kwa ufanisi.
“Mheshimiwa Rais umewahakikishia Watanzania hasa masikini jinsi unavyowajali maana mradi huu umewafikia zaidi ya wakazi milioni sita na hii inatokana na juhudi zako za kuendelea kuinua uchumi wa nchi,” amesema Waziri Mhagama
Aidha amemuhakikishia Rais kuwa fedha zote za tasaf zitawafikia walengwa kwa wakati na kwamba watasimamia kwa uadilifu kazi zote zinazotekelezwa katika mradi huo ambao unatarajia kulea matokeo chanya.
Mhagama ameongeza kuwa kutokana na uundwaji wa mifumo ya usimamizi pia watafanya uhakiki wa mara kwa mara utakaosaidia kuwatambua walengwa halisi wanaostahili kunufaika kwa wakati katika halmashauri zote 184 zilizopo nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa TAMISEMI David Silinde amesema kukabidhiwa kwa magari hayo kutasaidia kufuatilia maendeleo kwa jamii husika na kuongeza kuwa mradi wa TASAF umebadilisha maisha ya wanufaika.
Amesema jumla ya madarasa 13,000 yatajengwa katika shule za msingi na kwamba miradi 2400 imetoa ajira za muda kwa wanufaika na kuzikwamua kaya masikini ambapo shehia 388 zimefikiwa na mradi huo kwa upande wa visiwani Zanzibar.