Uongozi wa Azam FC umethibitisha taarifa za kukamilisha mazungumzo ya awali na kocha wa zamani wa Young Africans George Lwandamina, ambaye aliwasili nchini jana usiku akitokea kwao Zambia.

 Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdlkarim Amin amesema kuwa wamefanya mchakato wa kumleta kocha huyo baada ya kuukubali uwezo wake na wanaamini atakwenda sawa na sera yza klabu hiyo.

Amesema wanaamini taratibu nyingine za kukamilisha mpango wa kusaini mkataba na kocha Lwandamina zitakamilishwa kikamilifu, ili aweze kuanza kazi ya kuirudisha Azam FC kwenye ramani ya ushindani na kutwaa ubingwa msimu huu 2020/21.

“Kwa muda tulikuwa tunamfuatilia na tunatambua kwamba analijua soka la Bongo hivyo hatuna mashaka katika hilo, kikubwa mashabiki wawe pamoja nasi kazi bado inaendelea,” amesema.

Kwa upande wa kocha George Lwandamina amesema, amekuja ndani ya Azam FC kufanya kazi hivyo anatarajia ushirikino kutoka kwa viongozi, wachezaji pamoja na mashabiki.

“Nimefurahi kuja tena ndani ya Tanzania, nilikuwepo nikaondoka na sasa nimerudi tena, imani yangu ni kwamba tutakuwa pamoja katika kufikia mafanikio,” amesema.

Lwandamina anatarajiwa kuchukua nafasi ya kocha kutoka Romania Aristica Cioaba, ambaye alisitishiwa mkataba wake saa kadhaa baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans kati kati ya juma lililopita.

Wakati Lwandamina akiwasili nchini kuchukua mikoba ya Cioaba, kikosi cha Azam FC kipo jijini Mwanza kikijiandaa na mchezo wa Desemba 07 dhidi ya Gwambina FC, Uwanja wa Gwambina Complex ikiwa chini ya kaimu kocha msaidizi, Vivier Bahati.

Lwanga hadi Desemba 15
Rais wa Ufaransa ampongeza Rais Magufuli

Comments

comments