Mshambuliaji kinara wa timu ya Azam FC raia wa Zimbabwe, Prince Dube atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Yanga, Novemba 25 katika uwanja wa Azam Complex.
Dube alivunjika mfupa wa mkono wa kushoto na kutolewa dakika ya 18 ambapo Novemba 29 alipelekwa nchini Afrika Kusini katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town kwa ajili ya matibabu.
Msemaji wa Azam, Zaka Zakazi amesema baada ya nyota huyo kufika hospitali juzi, jana amefanyiwa vipimo na ikagundulika atakuwa nje kwa wiki sita kuuguza jeraha.
“Mshambuliaji wetu Prince Dube atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita baada ya matokeo ya vipimo alivyofanyiwa katika Hospitali ya Vincent Pallotti jana,” amesema Zaka.
Mpaka Dube anapatwa na majeraha hayo tayari alikuwa amefunga mabao sita na kwa sasa anazidiwa moja na kinara John Bocco wa Simba.