Mshambuliaji Rasmus Hojlund anatarajiwa kurejea mwishoni mwa juma hili katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest baada ya kukosa michezo miwili iliyopita.
Rasmus anatarajiwa kurudi na kuleta nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Erik ten Hag na taarifa zimeripoti atafanya mazoezi na kikosi kamili kuelekea mchezo huo.
Man United ilianza kususua na katika mechi mbili walizocheza walifunga bao moja tu lililowekwa kimiani na beki wa kati Raphael Varane huku safu yao ya ushambuliaji ikionekana butu.
Naye Ten Hag anaamini straika huyo mwenye umri wa miaka 20 atakuwa fiti asilimia 100 na huenda akawepo benchi kesho dhidi ya Nottingham Forest.
Chanzo cha habari kimeripoti kuna matarajio makubwa ya kuwepo kikosini kwa straika huyo, ambaye alitajwa na Ten Hag kama ni mshambuliaji wa aina ya kipekee.
Kauli hiyo aliisema baada ya kumfuatilia straika huyo kipindi anakipiga Atalanta katika msimu wake wa kwanza Serie A ambako alifunga mabao tisa.