Tajiri mtarajiwa kwenye kikosi cha Manchester United ameripotiwa kuwa na mpango wa kuwapiga Liverpool kwa kitu kizito kichwani kwa mchongo wake wa kumchukua mkali wao wa masuala ya usajili, Michael Edwards ili akapige kazi Old Trafford.

Mkurugenzi wa soka huyo wa zamani wa Liverpool amekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya kocha Jurgen Klopp huko Anfield.

Edwards alimsaidia kocha Mjerumani Klopp kwenye kunasa mastaa wake wa maana kabisa akiwamo mshambuliaji Mohamed Salah na beki wa kati kisiki Virgil van Dijk.

Aliachana na Liverpool, Mei 2022 na alikuwa akihusishwa na Real Madrid na Chelsea.

Lakini, ripoti zinafichua kwamba Edwards anaweza kurudi kwenye Ligi Kuu England na kwenda kufanya kazi Man United, jambo ambalo litawauma moyo sana mahasimu wao Liverpool.

Man United kwa sasa inaelekea kwenda kuwa chini ya bilionea wa Uingereza, Ratcliffe baada ya kuripotiwa kwamba huenda akamiliki asilimia 25 ya hisa za klabu hiyo.

Wamiliki wa sasa wa Man United familia Glazer wameripotiwa kujiandaa kukubali ofa ya Ratcliffe ya kumiliki aslimia 25 ya hisa za klabu hiyo kwa dau la Pauni 4 Bilioni. Makubaliano yaliyopo ni kwamba mmiliki huyo wa kampuni ya INEOS, Ratcliffe atajishughulisha zaidi na masuala ya soka.

Na kwenye hilo, kazi yake ya kwanza ya bilionea huyo ni kuajiri mkurugenzi mpya wa soka, ambaye atakuwa anasimamia masuala mbalimbali ya usajili.

Man United pia itatazama majina mengina na mojawapo yanayodaiwa kupewa nafasi kubwa na bosi Ratcliffe ni jina la Paul Mitchell, ambaye alifanya kazi na kocha Mauricio Pochettino walipokuwa pamoja Southampton na Tottenham.

Mitchell alifanya kazi pia na RB Leipzig na sasa ni mkurugenzi wa michezo wa klabu ya AS Monaco ya Ufaransa.

Dkt. Kikwete afurahia Wanawake kuupiga mwingi
Infantino, Motsepe kuwasili Dar es salaam