Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limewatoa wasiwasi wadau wa habari nchini baada ya ratiba ya Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea jijini Dodoma, kutotaja Muswada wa Sheria ya Habari.
Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile amewatia moyo wadau wa habari akisema amepokea taarifa kuwa muswada huo ungeingia bungeni muda wowote kuanzia jana, licha ya kutokuwa kwenye ratiba.
“Nina taarifa za uhakika kuwa, mpaka jana jioni kulikuwa na kila dalili kwamba Muswada wa Sheria ya Habari utaingizwa bungeni. Nimetoa taarifa hii sababu watu wengi wanaangalia ratiba ya bungeni wananipigia simu wanauliza ‘vipi mbona muswada haumo kwenye ratiba’?” amesema Balile.
Hata hivyo, Balile ameongeza kuwa anadhani Muswada wa Sheria ya Habari hautaingia bungeni na kujadiliwa kama ilivyo kwa Muswada wa Bima ya Afya, bali utaingia kwa mfumo wa mabadiliko madogo-madogo ya sheria mbalimbali (Miscellanea amendments).
Wadau wa habari wanasubiri faraja ya mabadiliko ya sheria inayosimamia tasnia ya habari, ili kuondoa vifungu wanavyoamini ni kandamizi na vinavyoongeza changamoto ya utoaji na upatikanaji wa habari.