Mabingwa mara nane wa kombe la ligi nchini England (ELC) Liverpool wamepangwa kuanza kampeni ya kusaka ubingwa wa michuano hiyo msimu huu kwa kupambana na Leicester City, ambao watakua nyumbani King Power Stadium.
Ratiba ya michuano hiyo imepangwa mjini Beijing nchini China mapema leo asubuhi kwa saa za Afrika mashariki.
West Bromwich Albion watanza michuano hiyo wakiwa nyumbani dhidi ya mabingwa mara nne Manchester City, Bournemouth watacheza dhidi ya Brighton and Hove Albion, na Crystal Palace watawakaribisha Huddersfield Town.
Manchester United, ambao waliichapa Southampton katika mchezo wa fainali msimu uliopita, wataanza kutetea taji lao kwa kucheza dhidi ya Burton Albion kwenye uwanja wa Old Trafford.
Mabingwa wa zamani wa barani Ulaya Nottingham Forest, ambao pia wamewahi kutwaa kombe la ELC mara nne watacheza dhidi ya Chelsea, baada ya kuivurumisha Newcastle Utd katika mzunguuko wa pili wa michuano hiyo kwa kuifunga mabao 3 kwa 2.
Mabingwa mara mbili wa ELC Wolverhampton Wanderers ambao waliifunga Southampton mabao 2 kwa 0 katika mzunguuko wa pili, wamepangwa kucheza na Bristol Rovers.
Mshambuliaji Chris Wood aliyejiunga na Burnley juma hili na kufanikiwa kucheza katika mchezo wa mzunguuko wa pili wa ELC dhidi ya Blackburn Rovers, atarejea tena kwenye klabu yake ya zamani ya Leeds United kwa ajili ya mchezo wa mzunguuko wa tatu.
Washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London Arsenal watakua nyumbani wakicheza dhidi ya Doncaster Rovers, huku mahasimu wao Tottenham Hotspur watalazimika kusubiri mshindi kati ya Derby County na Barnsley, baada ya kutoka sare kwenye mchezo wa mzunguko wa pili.
Michezo ya mzunguuko wa tatu ya ELC itachezwa Septemba 18 na 19.
Mdhamini mkuu wa michuano hiyo msimu huu ni Carabao Energy Drink, ambao makao yao makuu yapo China, na ndio maana ratiba ya mzunguuko wa tatu imelazimika kwenda kufanyika mjini Beijing.