Wawakilishi pekee wa England kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya Leicester City, watapambana na Atletico Madrid katika hatua ya robo fainali.
Leicester City, wamemfahamu mpinzani wao baada ya shirikisho la soka barani Ulaya kuendesha droo ya kupanga ratiba ya hatua ya robo fainali katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye ofisi za UEFA huko mjini Nyon nchini Uswiz.
Meneja wa muda wa Leicester City, Craig Shakespeare atakua na kazi ya kubuni mbinu mbadala kuipenya ngome ya Diego Simeone, huku akihakikisha safu yake ya ulinzi haipitiki kirahisi dhidi ya washambuliaji wa Atletico Madrid kwenye mchezo huo.
Ratiba ya michezo mingine inaonyesha kuwa, mabingwa watetezi Real Madrid watavaana na mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, huku mabingwa wa Italia Juventus wakipangiwa kuumana na FC Barcelona.
Borussia Dortmind watacheza dhidi ya wawakilishi kutoka nchini Ufaransa AS Monaco, ambao waliwatupa nje Manchester City usiku wa jumatano.
Zoezi la kuchezesha droo ya hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa limeendeshwa na mkurugenzi wa mashindano wa UEFA Giorgio Marchetti, kwa kushirikiana na Ian Rush ambaye ni balozi wa mchezo wa fainali wa utakaochezwa mjini Cardiff.