RB Leipzig imeweka ukomo wa hadi kufikia Agosti 12 kwamba mabosi wa Manchester City wawe wamekamilisha uhamisho wa beki wao, Josko Gvardiol mwenye umri wa miaka 21, la sivyo hawatawauzia.
Gvardiol ameripotiwa kuwa ameshafanya makubaliano binafsi na Man City tangu mwezi mmoja uliopita lakini kinachokwamisha dili lake ni kiasi cha pesa kinachohitajika na mabosi wa Leipzig.
Timu hii kutoka Ujerumani inahitaji walau Euro 100 milioni kumuuza Josko, dau ambalo litaenda kumfanya kuwa beki ghali zaidi katika histori ya soka barani Ulaya.
Ukomo wa usajili kwa Man City umewekwa mahususi kwa sababu kocha wa Leipzig anataka kutafuta mbadala wa Josko mapema, jambo ambalo linaweza kuwa gumu ikiwa fundi huyu atauzwa kwenye siku za mwisho za usajili.
Josko ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, ni miongoni mwa mastaa wanaohusudiwa sana na kocha wa Man City, Pep Guardiola ambaye alivutiwa naye zaidi kutokana na kiwango alichoonyesha kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka jana kule Qatar.
Leipzig hiyo Agosti 12 watakuwa wanacheza mechi ya German Super Cup.