Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ametakiwa kuhakikisha anawakamata Wafugaji wote wanaowapiga Wakulima na kulisha mifugo katika mashamba yenye mazao.
Agizo hilo, limetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki katika ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro ya Wakulima na Wafugaji aliyoifanya katika Wilaya za Kilwa na Liwale, mkoani Lindi.
Amesema, Wafugaji wengi hasa wanaohamahama kutafuta malisho wanalalamikiwa na Wakulima kuwa no chanzo cha uharibufu, ikiwemo matukio ya kuwapiga pindi anapotetea haki zao pindi wanapolisha mifugo katika mashamba yao.
“Vitendo vya ubabe vinavyofanywa na baadhi ya wafugaji havikubaliki, nchi haiwezi kuwa na jamii ya namna hiyo, na hivyo wale wote wanaofanya vitendo hivyo hawatavumiliwa,” amesema Waziri Ndaki.
Waziri huyo wa Mifugo amebainisha kuwa, “Mkuu wa Mkoa na timu yako naomba wale wote wanaolisha mifugo katika mashamba ya wakulima wakamatwe kuanzia leo hii wawekwe ndani na wafunguliwe mashtaka.”
Kufuatia agizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amewaelekeza Wakuu wa vituo vya Polisi katika Wilaya ya Kilwa na Liwale kuwakamata wafugaji waliowapiga wakulima na kwamba apatiwe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo.
Rais aonja chungu ya Mahakama, awekewa vikwazo
“Yupo kijana alimpiga diwani hapa Kata ya Kimambi, hiyo ni dharau na haikubaliki nakuagiza OCD upo hapa nataka uondoke na huyo aliyemlipa diwani, na wale wote wanaohusika na vitendo hivyo wakamatwe leo,” ameagiza Telack.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki aliwataka Wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la kusajili mifugo yao, huku akiwahimiza kuanza kumiliki maeneo yao ya kufugia hali itakayosaidia kupunguza migogoro.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwataka Watendaji wa Kata na Wenyekiti wa vijiji kujitafakari kwa sababu baadhi yao wanalalamikiwa kuwa sio waadilifu na kuwa ni sehemu ya migogoro hiyo.