Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili na kuhimiza wasimamizi elimu ya sekondari kuacha tabia ya wizi wa mitihani .

Kunenge ameyasema hayo katika kikao kazi kilichowakutanisha baadhi ya walimu kutoka kata mbalimbali za manispaa ya Ilala pamoja na watumishi kutoka ngazi ya manispaa kwa kutambua changamoto na jitihada kubwa zilizofanywa na waalimu.

“Nitumie fursa hii kuwapa onyo walimu hasa shule za sekondari wanaoungana na wamiliki wa shule kuiba mitihani ama kufanya udanganyifu wowote hiyo tabia iache mara moja haitavumilika,” amesema Kunenge.

Aidha Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha anatoa kipaombele cha ajira kwa walimu ili kuweza kukidhi changamoto ya uhaba wa walimu kwa baadhi ya shule.

Naye mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri ametoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato amesema zaidi ya bilioni 58 zimekusanywa huku manispaa hiyo ikizidi kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo.

Kwa upande wao walimu waliohudhuria katika mkutano huo wamesema vikao kazi ndo msingi wa ufanisi kwa kuwa hukumbusha majukumu kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuwasilisha changamoto wanazokumbana nazo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 23, 2020
Fursa soko la korosho nchi za nje