Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amezindua Barabara za Mkwajuni Kata ya Mbweni zenye urafu wa Kilomita 7.85 ambazo ujenzi wake umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 12, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha za Ujenzi wa Barabara hiyo ambayo imekamilika kwa asilimia 100.
Makalla amezindua Barabara hiyo Mei 04, 2023 na kusema licha ya Kata ya Mbweni kuonekana ya kisasa kama zilivyo kata zingine zilizopiga maendeleo, pia Wananchi wataondokana na adha ya changamoto ya ubovu wa miundombinu ya Barabara hasa tatizo la mafuriko nyakati za msimu wa Mvua za masika.
Amesea, “kipekee naomba nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuidhinisha fedha za Ujenzi wa Barabara hii katika Kata ya mbweni ambayo imekamilika kwa asilimia 100 na kuifanya Kata ya Mbweni kuwa ya kisasa kama Masaki.”
Kufuatia kukamilika kwa Barabara hiyo, Makalla amempongeza Mkandarasi King’s Builders kwa kukamilisha Ujenzi wa Barabara hiyo na kuikabidhi kwa wakati ikiwa kwenye ubora mzuri kwa mujibu wa mkataba alio saini na Serikali.
Katika hatua nyingine, Makalla ametoa wito kwa Wananchi wa Mbweni kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya Barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kutotupa taka kwenye mitaro, kutoharibu taa za Barabarani na kila nyumba kupendezesha mbele ya majengo kwa kuweka bustani.