Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amesema ifikapo wiki ya pili ya mwezi October wapenzi wa burudani Jiji humo wanatarajiwa kuelekea Coco Beach kushuhudia mwonekano mpya na wa Kisasa wa eneo hilo kupitia Tamasha la DAR SUNSET CARNIVAL litakalohusisha burudani za aina mbalimbali.
Mapema leo RC Makalla amefika kwenye eneo hilo maarufu kwa uuzaji wa mihogo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyotoa ya kuboresha mandhari ya ufukwe huo ambapo tayari Wadau kutoka Kampuni zote za Vinywaji ikiwemo Coca cola, Pepsi, Azam Bakhresa, ASAS na Bank za NMB na CRDB zimejitolea kuwajenja Wafanyabiashara hao Vibanda vya kisasa bure.
RC Makalla amesema lengo la Serikali ni kuona eneo hilo linakuwa sehemu nzuri ya utalii wa fukwe ili kuwezesha wananchi wote kupata sehemu ya mapumziko na familia na kuchochea biashara Jambo litakalosaidia pia Makusanyo ya Mapato.
Aidha RC Makalla amesema Miongoni mwa burudani zitakazopatikana eneo hilo ni Burudani ya Mziki, Maonyesho, michezo ya watoto, Gari la kipekee lenye Club, Gari la Kisasa la mziki, utalii wa boti, na pia upatikanaji wa Vyakula na Vinywaji.
Hata hivyo RC Makalla amesema tayari ameelekeza Vyombo vya ulinzi na usalama Kuimarisha ulinzi kwenye eneo hilo.