Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla leo ameongoza kikao Cha Kamati ya ushauri ya Mkoa RCC kuhusu mapendekezo ya bajeti ya Mkoa huo kwa Mwaka wa fedha 2022-2023 ambapo Mkoa huo umeomba kupatiwa kiasi Cha Shilingi bilioni 650.97 kwaajili ya utekelezaji wa Shughuli mbalimbali ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 88.7 kwa Mwaka 2021/2022.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, RC Makalla amesema kiasi hicho kinajumuisha Mishaha Shilingi Bilioni 338.2, Miradi ya maendeleo Shilingi Bilioni 77.7 na Matumizi mengine kiasi Cha Shilingi bilioni 10.8 ambapo upande wa makusanyo Mkoa umelenga kukusanya Shilingi Bilioni 224.
Aidha RC Makalla amesema miongoni mwa vipaombele vitakavyozingatiwa ni pamoja na kudumisha amani, ulinzi na usalama, Ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kuboresha Elimu, Afya, Mazingira Bora ya Biashara, miradi ya kimkakati, ustawi wa jamii, kudhibiti na Kupunguza Majanga.
Ili kuhakikisha Serikali inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, RC Makalla ametoa wito kwa Halmashauri kuhakikisha zinasimamia kikamilifu makusanyo ya mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Kikao hicho pia kwa kauli moja kimeazimia kumpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jijini humo pamoja na kutoa fedha kwa wakati jambo linalosababisha miradi kutekelezeka kwa wakati pasipo usumbufu wowote.