Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ameunga mkono hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gellasius Byakanwa kuondoa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la Kilimanjaro Veggie linalomilikiwa mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, RC Mghwira amesema kuwa hatua hiyo inatokana na uzingatiaji wa sheria na haikua na malengo ya kisiasa. Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mazingira, hairuhusiwi kufanya shughuli za binadamu umbali wa mita 60 kutoka katika chanzo cha maji, sheria ambayo ilikuwa imekiukwa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa awali Mbowe alikiri kuvunja sheria na kukubali kuwa angeondoa miundombinu yake na mazao ndani ya shamba hilo kwa muda wa miezi minne (hadi Mei 23), lakini hakufanya hivyo na badala yake aliongeza mazao mengine.
“Yeye ni kiongozi angetusadia kuelimisha wananchi kuhusu kuheshimu sheria lakini amekuwa wa kwanza kuzivunja na serikali imeweka sheria ya mita 60 kusifanyike shughuli za kibiadamu ,”alisema.
Alisisitiza kuwa mmiliki wa shamba hilo ameshakiri kufanya kosa na kukubali kulipia fidia ya shilingi milioni 18, hivyo zoezi la kuondoa miundombinu kwenye shamba hilo inapaswa kuendelea.