Serikali Mkoani Tabora imewakabidhi watoto wawili waliokuwa wamepotea mkoani Mbeya kwa wazazi wao wakiwa na afya njema.

Akikabidhi watoto hao jana Mkuu wa mkoa wa Tabora alitoa onyo kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya aina hiyo ikiwemo kuiba watoto wachanga na kusema kwambaSerikali itahakikisha inawachukilia hatua kali za kisheria.

Hatua hiyo imetokana na kupatikana mmoja wao akiwa na mwanamke mmoja Hawa Ally katika Hospitali ya wilaya ya Nzega baada ya wasamalia wema kuwa na wasiwasi na mtuhumiwa na kutoa taarifa polisi.

Mwanri amewashukuru wananchi, Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wao waliouonyesha na kupelekea kupatikana kwa watoto hao wakiwa na afya njema.

Baba mzazi wa watoto hao ambaye ni mtumishi katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Mashaka Juma amesema watoto wake walipotea mnamo Desemba 28, mwaka jana.

Amesema mtoto wake mmoja mwenye miaka mitano na mwingine mwenye mwaka mmoja na nusu walipotea wakati yeye na mkewe wakiwa wamekwenda sokoni kunua mahitaji na waliporudi ndipo walipobaini hawapo nyumbani kwao.

Yeye pamoja na mkewe wametoa shukurani kwa vyombo vya habari, polisi na uongozi wa mkoa wa Mbeya na Tabora kwa kufanikisha watoto wao kupatikana japo kwao bado ni kama ndoto kuwapata watoto wao wakiwa hai.

Ofisa ustawi wa jamii mkoa wa Tabora, Baraka Makona, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alimuacha mtoto mkubwa kwenye nyumba ya mkazi wa chemichemi kwa madai anaenda kupeleka mdogo hospitali na kuahidi kurudi baadaye.

Amesema mtuhumiwa hakurudi siku hiyo mwishoni mwa mwaka jana, jambo lililomfanya mwananchi aliyetelekezewa mtoto kutoa taarifa Polisi.

Hivyo baada ya ofisi za mkuu wa mkoa kupata taarifa za kupotea kwa watoto hao, walifuatilia na kugundua mtoto mkubwa katelekezwa Manispaa ya Tabora na mdogo alipatikana mjini Nzega.

Mwandishi aliyetekwa miaka mitatu Syria aachiwa huru
Video: Mzee Manara azifunda Simba, Yanga awakumbuka Makambo, Okwi