Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen ameishauri benki ya NMB kufungua tawi katika bonde la Ziwa Rukwa ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi ambao shughuli zao kubwa za kiuchumi ni kilimo cha mahindi, mpunga pamoja na uvuvi.

Zelote ametoa ushauri huo katika ufunguzi wa siku ya huduma kwa wateja iliyofanywa na benki ya NMB kanda ya nyanda za juu katika Kijiji cha Mfinga, kata ya Mfinga, Wilaya ya Sumbawanga, kabla ya kukabidhi vifaa vya shule pamoja na hospitali vyenye thamani ya Shilingi milioni 20.

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutaepusha matukio ya uvamizi na mauaji yanayofanywa na baadhi ya watu wanaowavizia wakulima na wafanyabiashara wanaoweka fedha majumbani mara tu baada ya mauzo ya mazao yao.

“Mimi nashauri Benki ya NMB muwe na Tawi huku, si lazima kuwa na jengo, hata ile Mobile Banking ambayo mwananchi anaweza kupata huduma zote za kuweka na kutoa fedha katika gari hiyo, ili fedha zao hawa ziwe katika mikono salama,” amesema Zelote.

Sambamba na hilo Zelote amewahamasisha wakulima pamoja na wafanyabiashara wa Kata ya Mfinga kufungua akaunti benki na pia kujiunga katika vikundi ili kuwa na urahisi wa kupata mikopo  na kuweza kuwainua kiuchumi.

“Mbali na kuhifadhi fedha pia benki inatoa mikopo kwaajili ya kujiendeleza na hatimae kuwainua wakulima waweze kuongeza thamani ya mazao yao na kupata soko pana hasa katika awamu hii inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli inayohamasisha uchumi wa viwanda kwa taifa,” Alisema.

Amewataka viongozi wa Kijiji na wanufaika wa vifaa hivyo kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kuwahudumia wananchi bila ya bugudha na kuonya kuwa wananchi wasiogope kuwashitaki watumishi wanaowahudumia kwa viburi.

 

Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 4, 2017
Chama cha CCK chapanga kufanya mkutano mkuu Ikulu