MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewaagiza viongozi wa mitaa, vijiji na kata kwa ushirikiano na mawakala wa sensa kuhakikisha wanawaandaa wachimbaji wadogo ili kufanikisha zoezi la sensa kwenye maeneo ya migodini.
Shigella ametoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumuza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani hapa pamoja na mawakala wa sensa wilayani humo wanaoendelea na semina kuelekea zoezi la sensa.
Amesema mkoa wa Geita una maeneo mengi ya wachimbaji wadogo hivo ni lazima uandaliwe utaratibu mzuri wa mapema ili kuepuka sintofahamu pindi mawakala wa sensa watakapowasili kutekeleza majukumu yao.
“Ni vizuri watendaji wetu wa vijiji na kata pamoja na madiwani, tufanye maandalizi mapema kwenye yale mazingira, maana usipowaandaa wachimbaji wadogo, ukaenda saa sita usiku kwenye machimbo unawaambia nimekuja kuwahesabu sensa hawatakuelewa.