Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, huenda ikaingia matatani baada ya kudaiwa kupokea zaidi ya Sh.milioni 600 za wananchi ambao waliwahidi kuwapatia mashamba ya kulima korosho lakini ni miaka minne sasa hawajagawiwa maeneo hayo.
Kufuatia malalamiko ya wananchi waliotoa fedha hizo kwa kuziweka kwenye akaunti maalumu ya halmashauri kama walivyokuwa wameelekezwa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge aliitisha kikao cha kamati tendaji ya mradi wa korosho Manyoni mkoani hapa juzi.
Mkuu wa Mkoa Dk.Mahenge ameagiza kamati hiyo hadi kufika Jumatatu ya Januari 17 mwaka huu iwe imetoa taarifa ya mradi huo iliyosahihi ambayo itapitiwa kwanza na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kabla ya kuwasilishwa kwake.
Dk.Mahenge ameagiza kuandaliwa upya kufuatia taarifa iliyokuwa ikitolewa kutojitosheleza kwani majina ya baadhi ya watu wanaodaiwa kulipia fedha hayakuwepo licha ya yeye kuwa nayo huku kiasi cha fedha kilichopokelewa kikiwa hakijabainishwa.
“Taarifa hiyo muiandae vizuri najua hizo namba mnazo nendeni mkaziunganishe na muwe makini kama kuna watu walikuwa wakiingiza fedha hizo benki mnapaswa kuwajua, wapo walioleta fedha hizo ofisini, mliowapa mashamba, ambao bado hamjawapa, waliopanda au kupalilia hivyo nawaombeni tengenezeni taarifa inayojitosheleza,” alisema Dk. Mahenge.
Alisema haiwezekani mkapokea fedha za mtu halafu mkashindwa kuandaa taarifa kwani jambo hilo sio geni kwao na kama taarifa hiyo inashindwa kuandaliwa vizuri patakuwa na kizungumkuti hamna taarifa hizo huenda zitakuwa kwa mtu mmoja bila kushirikishwa wengine na hawajui lakini kama wajumbe wote wa kamati hiyo wangekuwa wanajua isingeshindwa kuandaliwa.
“Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya nawaombeni taarifa hii ikaandaliwe upya ili tupate uwazi taarifa ioneshe toka mlipoanzisha mradi huu mlitenga eneo kiasi gani, watu wangapi walioleta maombi na kulipa, masharti yenu yalikuwaje, gharama za usafiri ilikuwa ni shilingi ngapi, gharama za fomu, michango iliyotolewa kama zahanati na mingine ilikuwa kiasi gani na barabara vitu vyote viahinishwe na ioneshe fedha mlizopokea kama zipo sawa na zile zilizopo benki na kama zipo ambazo mlizipokea na hamkuzipeleka benki pia mzioneshe,” amesema Dkt.Mahenge.
Aidha amesema taarifa hiyo pia ioneshe fedha zilizopokelewa kama mashamba yake yapo kwani kuna uwezekano wa fedha zilizoingizwa zikawa ni zaidi ya ekari za mashamba walizonazo hivyo waeleze kuwa kutokana na kutofunga akaunti walipokea fedha hizo ili kama kutakuwa na uwezekano watu hao ambao watakosa maeneo watafutiwe sehemu nyingi kama Itigi au Ikungi kwa makubaliano kwa sababu shida yao ni kupata mashamba.
Naye Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Manyoni ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo Aderaide Rweikiza alisema taarifa kamili ya mchakato wa mradi huo tangu kuanza kwake na matumizi yote ya fedha ipo na kuwa wataiwasilisha kwake mkuu wa mkoa.