Mmiliki wa Kiwanda cha Maziwa cha Tabora amepewa mwezi mmoja kuhakikisha kuwa anarekebisha kasoro zote zilizosababisha kiwanda hicho kufungiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa TFD mwaka 2016 vinginevyo Serikali itakichukua na kumpa mtu mwingine ili akiendeshe.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Tabora, Aggrey Mwanri mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea Kiwanda hicho ili kujionea mazingira yaliyosababisha kiwanda hicho kisimamishwe.
Amesema kuwa mara baada ya kipindi cha mwezi kukamilika na kama Mmiliki wake atakuwa hajarekebisha mapungufu aliyoelekezwa na TFDA ayafanyie kazi itabidi apeleke mapendekezo katika Wizara inayohusika ya Viwanda ili kikabidhiwe kwa mwekezaji mwingine.
Aidha, Mwanri ameongeza kuwa sanjari na kumwagiza alerekebishe kasoro pia amemtaka apeleke Mkataba wa Ununuzi wa Kiwanda hicho ili kuona kama anazingatia masharti aliyopewa wakati akikinua mwaka 1998.
Kwa upande wa Meneja wa Kanda ya Magharibi wa TFDA, Dkt. Edgar Mahundi amesema kuwa walipofanya ukaguzi katika kiwanda hicho walikuta maziwa yakizalishwa katika mazingira ambayo ni hatari kwa afya ya watumiaji.
Hata hivyo, Dkt. Mahundi amongeza kuwa jambo jingine aliagizwa kuhakikisha kuwa anakuwa na maabara na wataalam wa kutoka katika Kiwanda chake lakini ameshindwa kutekeleza maagizo hayo.