Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameshauri jeshi la magereza kuhakikisha wanazitumia ekari 11,000 zinazomilikiwa na jeshi hilo kwa ajili ya mazao ya alizeti pamoja na kahawa ili jeshi hilo liweze kujipatia fedha na kutatua changamoto mbalimbali walizonazo na kuongeza uzalishaji wa mazao hayo katika taifa.
Amesema kuwa nchi ya Tanzania huagiza asilimia 60 ya mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi wakati jeshi la magereza lina ardhi nzuri na ya kutosha kwaajili ya kuzalisha zao la alizeti kwa wingi na hatimae kupunguza uwingi wa mafuta unaoagizwa kutoka nje na kuokoa mabilioni ya fedha yanayotumiwa na serikali katika kununua mafuta hayo.
“Pamoja na kuinua uchumi lakini pia tunaweza kulisha nchi yetu kwa mafuta, sisi mkoa wa Rukwa tupo katika hali nzuri ya kulima alizeti na kuchangia kupunguza pengo la mafuta yasiendelee kuagizwa kutoka nje, tumejipanga kama Mkoa, karibu kila kaya inayolima iweze kuwa na angalau ekari moja ya alizeti, na kwenye majeshi yetu hapa mna ekari hizi 11,000 mnaweza kuzalisha na kupata ekari za kutosha kutatua changamoto mlizonazo,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa kuanzia jeshi hilo linaweza kutumia ekari 1000 kuanza kulima na kuona mafanikio yake ndani ya mwaka mmoja kwani kwa mujibu wa Great African Food Company (GAFCO) wanaofanya kilimo cha mkataba hununua kilo moja ya alizeti kwa shilingi 900 huku gunia moja likiwa na kilo 70 na kila ekari moja hupata gunia zisizopungua 15 matokeo yake tunaweza kupata 945,000,000/= na kuwataka magereza kushirikiana na GAFCO ili kufanikisha zozi hilo.
Ameyasema hayo alipofanya ziara fupi katika gereza la Mollo lililopo katika kata ya Mollo, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ili kujionea miradi ya maendeleo ya gereza hilo linalomiliki ekari 11,000 huku wakitumia ekari 400 kwaajili ya kilimo cha mahindi na maharage pamoja na uzalishaji wa mbegu za mahindi.
Kwa upande wake akisoma risala ya gereza Mkuu wa Gereza la Mollo, ACP John Mwamgunda amesema kuwa gereza hilo limekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo uchakavu wa vifaa vya kilimo, sare za wafungwa na majengo amabyo ni ya siku nyingi lakini alikubali kuwa uzalishaji wa alizeti ni rahisi zaidi ukilinganisha na uzalishaji wa mahindi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji, Tanzania hutumia Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya kula nje ya nchi huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za mafuta hayo tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa bidhaa hiyo kwa mwaka.