Mashabiki wa soka wa klabu ya Valencia, mara kwa mara wamekua wakionyesha mapenzi na timu yao na msimu huu wanatarajiwa kuujaza uwanja wa Mestella pindi timu yao itakapokua na kibarua kigumu cha kuwakabili Real Madrid, mishale ya saa tano kwa saa za Afrika mashariki.

Uwanja wa Mestalla unatarajiwa kufuruka katika mchezo wa jumapili, kama ilivyokua wakati timu hizo zilipokutana kwa mara ya kwanza Disemba 25 mwaka 1932.

Real Madrid wataingia uwanjani wakiwa katika kiwango bora, na mpaka sasa wameshavuna alama 16 katika michezo 18 iliyopita, wamefunga mabao 16 huku wakifungwa mabao mawili pekee. Wenyeji Valencia nao wamekua na kiwango cha kupambana na wamejitahidi kukwea hadi kwenye nafasi ya saba katika msimamo wa La Liga, wakichagizwa na ushindi katika michezo minne miongoni mwa michezo mitano iliyopita.

Mshambuliaji hatari na wa kutumainiwa wa Los Blancos (Real Madrid) Karim Benzema alionekana kuwa mwiba mkali katika mchezo uliopita dhidi ya Espanyol walipotembelea Estadio Santiago Bernabeu mwishoni mwa juma lililopita, akifunga bao la pili, huku akimtengenezea mfaransa mwenzake Raphael Varane, aliefunga bao la kwanza na kufanikiwa kunyakua alama tatu muhimu za mtanange huo.

Vijana Fede Valverde na Rodrygo Goes wamekua kivutio kikubwa kwenye kikosi cha Los Blancos na siku ya jumapili wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Zinedine Zidane, ambaye anahitaji kushinda mchezo dhidi ya Valencia.

Kwa upande wa Valencia ambao walionyesha ukakamavu katika mchezo uliopita kwa ushindi wa mabao manne kwa mawili dhidi ya Levante juma lililopita, nao watahitaji kushinda nyumbani dhidi ya Real Madrid.

Kevin Gameiro ambaye alionekana kuwa mwiba mkali katika mchezo uliopita dhidi ya Levante anatarajiwa kuwa kiongozi mzuri katika safu ya ushambuliaji akisaidiwa na kinda lenye miaka 19 Ferran Torres aliefunga bao la tatu katika ushindi wa mabao manne kwa mawili.

Kikosi cha Albert Celades (Valencia) kinajivunia rekodi ya kutopoteza mchezo kwenye uwanja wao wa nyumbani katika michezo minane kwa msimu huu. Kwa mara ya mwisho waliwafunga wapinzani wao Villareal uwanjani hapo mabao mawili kwa moja, huku timu nyingine zilizoondoka na vichapo kwenye uwanja wa Mestella kwa siku za karibuni zikiwa ni Granada na Alaves.

Nahodha wa Valencia Dani Parejo na Ezequiel Garay jumapili watakua wakicheza dhidi ya klabu iliyowakuza, huku kiungo mchezeshaji wa Real Madrid Isco atarejea Estadio Mestella ambapo alikuzwa kwa muda wa miaka saba, kabla ya kuanza kucheza katika ligi ya Hispania Novemba 2010.

Michezo mingine ya ligi ya Hispania (La Liga) itakayochezwa jumamosi

Granada Vs Levante

Real Sociedad Vs Barcelona

Athletic Bilbao Vs Eibar

Atletico Madrid Vs Osasuna

Michezo ya La Liga itakayochezwa jumapili.

Getafe Vs Real Valladolid

Celta Vigo Vs Mallorca

Espanyol Vs Real Betis

Sevilla Vs Villarreal

 

Makamba, Kinana, Membe kikaangoni, Kizungumkuti usajili laini za simu
Tanzania, Kenya zaahidi kuendeleza na kukuza maendeleo