Wabishi wa mji wa Madrid (Real Madrid) huenda wakabadili mawazo ya usajili wa malinda mlango, kufuatia figisu figisu walizoanza kuziona kuhusu mpango wa uhamisho wa Thibaut Courtois wa Chelsea.
Madrid wamejizatiti kuifanya maboresho nafasi ya ulinzi wa lango, kwa kumsaka mtu ambaye atakidhi haja ya kusimama langoni kwa kujiamini wakati wote ili kutunza hadhi ya klabu hiyo.
Tayari wameshaanza kuona dalili za kushindwa katika jaribio la usajili wa mlinda mlango wa vinara wa ligi ya nchini England (Chelsea) Thibaut Courtois, ambaye amekua chaguo lao la kwanza katika harakati zao itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa zinadai kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kusitishwa kwa mpango wa kumfuatilia mlanda mlango huyo, ambaye aliwahi kuwatumikia mahasimu wao Atletico Madrid kwa mkopo akitokea Chelsea kuanzia mwaka 2011-2014.
Mbadala wa mlinda mlango huyo kutoka nchini Ublegiji anatajwa kuwa Hugo Lloris, ambaye kwa sasa ni mali halali ya klabu ya Tottenham Hotspurs.
Hata hivyo bado kuna changamoto za kufanikisha mpango huo, kutokana na Lloris, mwenye umri wa miaka 30, kuwa na mkataba wa muda mrefu na Spurs ambao aliusaini mwishoni mwa mwaka jana.
Lakini pamoja na changamoto hiyo, bado Real Madrid wanaamini ushawishi wa kumpata mlinda mlango huyo, ambaye aliwahi kuitumikia klabu ya Olympique Lyon ya nchini kwao Ufaransa utakua rahisi, tofauti na kwa Courtois ambaye anaonekana kuwa tegemeo kubwa la Chelsea.
Real Madrid kwa sasa imekua ikimtumia mlinda mlango kutoka Costa Rica Keylor Navas kama chaguo la kwanza akisaidiana na Kiko Casilla.