Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Eden Hazard ameingizwa kwenye orodha ya wachezaji watakaoachwa na Real Madrid, katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa.
Taarifa zilizoripotiwa na gazeti la The Marca la Hispania zimeeleza kuwa, Mabosi wa klabu hiyo ya mjini Madrid wameafikiana kuuzwa kwa kiungo huyo aliesajiliwa misimu miwili iliyopita akitokea Chelsea ya England kwa Pauni milioni 130.
Jambo kubwa linalotoa msukumo kwa Hazard kuingizwa kwenye orodha ya watakaoondoka Santiago Berbabeu, ni kushindwa kwa mchezaji huyo kuonesha uwezo wa kisoka kama alivyotarajiwa.
Mpaka sasa Hazard ameitumikia Real Madrid katika michezo 43 za michuano yote na kufunga mabao matano. Kiwango ambacho ni chini ya malengo yaliyowekwa wakati akisajiliwa mwaka 2019.
Kiungo huyo ambaye pia ni Nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji aliwahi kusema anatamani kurudi Chelsea, lakini hadi sasa klabu huyo haijaonesha nia yoyote ya kumsajili kwa mara ya pili.