Klabu ya Soka ya Real Madrid imethibitisha kifo cha Farid, ambaye ni kaka wa kocha wa klabu hiyo na mwanasoka nguli, Zinedine Zidane.

Uongozi wa klabu hiyo umeeleza kuwa Zidane amepewa likizo fupi. Imeelezwa kuwa kaka yake alifariki akiwa na umri wa miaka 54 kutokana na ugonjwa uliokuwa unamsumbua kwa muda mrefu.

Mtoto wa Zidane, Luca ambaye ni mlinda mlango wa klabu hiyo pia aliambatana na baba yake Ijumaa, Julai 12, 2019 kutokana na kupokea taarifa hiyo ya msiba.

Real Madrid ilithibitisha kifo cha Farid kupitia tovuti yake huku ikitangaza kuwa katika mazoezi yanayoendelea ya klabu hiyo kutakuwa na wakati wa ukimya kwa ajili ya kumkumbuka na kumuombea.

“Wachezaji wetu wote walikuwa na wakati wa ukimya kuelekea katika kambi ya mazoezi, Montreal kufuatia kifo cha Farid Zidane, kaka wa kocha wetu mkuu, Zinedine Zidane,” imeeleza taarifa hiyo.

Kocha msaidizi, David Bettoni ataiongoza timu hiyo katika mazoezi hadi Zidane atakaporejea.

Wawili hao ni marafiki wa karibu. Walikutana kwa mara ya kwanza walipokuwa wanacheza katika timu ya vijana nchini Ufaransa.

Chadema watangaza kutinga mahakamani kudai ubunge wa Lissu
Wanawake 11 wakamatwa kwa kurekodi filamu za ngono