Klabu ya Real Madrid imekanusha kufanya mazungumzo na Kylian Mbappe kuhusu kumnunua Mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain msimu ujao wa majira ya joto.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’, ilikanusha ripoti iliyosema kwamba mazungumzo yamefanyika na kusema ni “uongo kabisa” katika taarifa iliyotolewa.
“Mbele ya habari zinazotangazwa na kuchapishwa na vyombo mbalimbali vya habari, ambavyo vinakisia kuhusu mazungumzo yanayodhaniwa kuwa kati ya mchezaji Kylian Mbappe na klabu yetu, Real Madrid inataka kusema kwamba habari hizi ni za uongo kabisa na mazungumzo yaliyosemwa na mchezaji ambaye ni wa PSG hayajafanyika,” ilisema taarifa ya Real Madrid.
Gazeti la Marca katika habari yake ya ukurasa wa mbele Alhamisi liliripoti kwamba “Madrid wanakaa kimya, lakini klabu inamwona akiwa amevaa nguo nyeupe mwaka 2024.”
Gazeti la Ufaransa L’Equipe liliandika Ijumaa (Novembe 03) kwamba Madrid “bado wanamngoja Mbappe,” wakati Jumamosi (Novemba 04) Diario AS iliripoti kwamba fowadi huyo angetarajia kupata euro milioni 35 kwa mwakani akitua Bernabeu.
Mbappe amekuwa akilengwa sana na Madrid na rais wa klabu Florentino Perez kwa muda mrefu.
Miamba hao wa La Liga walishindwa kumsajili Mbappe mwaka 2021 walipowasilisha ofa ya euro milioni 200 siku ya mwisho ya uhamisho, ambayo ilipuuzwa na PSG na mwaka 2022, wakati walikuwa karibu kumpata kwa uhamisho wa bure kabla ya yeye kuamua kusaini mkataba mpya Paris.
Madrid walihusishwa tena na Mbappe msimu uliopita wa majira ya joto alipotangaza kwamba hatasaini nyongeza ya PSG, ikimaanisha kuwa atakuwa huru kufanya mazungumzo na klabu nyingine Januari 2024 kabla ya kuhama msimu wa maji ya joto.
Klabu hiyo ya Hispania iliacha jezi namba tisa ikiwa wazi kwa msimu wa 2023-24 na badala yake wametegemea mabao ya Jude Bellingham.
Mbappe amefunga mabao 10 katika mechi 10 za Ligue 1 akiwa na PSG hadi sasa msimu huu, na mawili katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Ulaya.