Klabu ya Real Madrid imepanga kumuunganisha Kylian Mbappe kwenye kikosi chake katika msimu huu wa kiangazi endapo itapata upenyo wa kuachana na Gareth Bale, kwa mujibu wa Don Balon.
Madrid imekuwa na kiu ya kumnyakua Mbappe anayetazamwa kama Cristiano Ronaldo au Lionel Messi wa siku za usoni, lakini mtihani mkubwa ni uwepo wa Bale na kitita anachochota kwenye timu hiyo.
Inaelezwa kuwa Bale yuko mguu pande na mguu sawa kutaka kuachana na Real Madrid wakati wowote hali inayompa nafasi zaidi Mbappe kupenya kwenye kikosi hicho.
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Tottenham amemshauri Bale kuachana na Real Madrid kutokana na hali inayoonekana hivi sasa ya kulaumiwa kwa kila kipigo wanachopata.
“Bale anaonekana kulaumiwa kwa kila kitu kinachoenda vibaya ndani ya Real Madrid, kitu ambacho sio sahihi. Katika msimu huu amepata magoli 12 kwenye michezo 30, anafanya vizuri lakini bado analaumiwa. Kama unajisikia haukubaliki, unapaswa kuondoka,” alisema Berbatov kwenye mahojiano maalum na Betfair.
“Ni suala la pesa tu, sidhani kama Tottenham wana uwezo wa kulipa mamia ya mamilioni ya dola kwa mchezaji mmoja. Lakini Bale ni mchezaji wa kiwango cha juu duniani na itakuwa vizuri kwake kurejea kwenye Ligi Kuu,” aliongeza.
Robert Pires alimtaja Mbappe kuwa mchezaji ambaye ana nafasi ya kushinda Ballon d’Or siku za usoni.
Jana, Real Madrid ilipokea kipigo kibaya cha 4-1 dhidi ya Ajax kwenye Ligi ya Mabingwa.