Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Brazil, Vinicius Junior amesaini dili jipya la kuendelea kuitumikia Real Madrid hadi 2027, imeelezwa.
Baada ya kufurahia vyema kabisa msimu wake wa kwanza 2021-22 alipokuwa na uzi wa Los Blancos, Vinicius ameendelea kuwa mchezaji muhimu kabisa kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Carlo Ancelotti.
Vinicius alimaliza msimu uliopita wa 2022-23 kwa kufunga mabao 23 na asisti 21 katika mechi 55 za michuano yote, akiisaidia Real Madrid kushinda Klabu Bingwa Dunia, Copa del Rey na UEFA Super Cup.
Hata hivyo, Los Blancos ilikumbana na wakati mgumu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga, huku Vinicius mwenyewe akijikuta akikabiliwa na masuala ya kibaguzi, alipokwenda kukipiga na Valencia uwanjani Mestalla, Mei.
Katika mkataba huo wa miaka minne aliongeza Mbrazili huyo wa kuendelea kubaki Santiago Bernabeu, Real Madrid imeweka kipengele cha kuhitaji ilipwe Euro 1 bilioni kwa timu yoyote itakayotaka kuvunja mkataba wake na kumsajili.
Los Blancos imepanga kutangaza dili hilo la kumwongezea mkataba Vinicius wakati wachezaji wote watakaporejea kutoka likizo, huku Mbrazili huyo akiwamo kwenye orodha ya wachezaji walioongezewa likizo.
Real Madrid ililipa Euro 45 milioni kunasa saini ya mchezaji huyo kutoka Flamingo ya Brazil mwaka 2018, wakati huo alipokuwa na umri wa miaka 18.
Kwa jumla wake, kwenye kikosi cha Real Madrid, Vinicius amefunga mabao 59 na asisti 64 katika mechi 225.