Rais wa Klabu ya Real Madrid, Florentino Perez, amekiri kuwa anataka kumsajili Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na Klabu Bingwa nchini humo PSG Kylian Mbappe.
Mshambuliaji huyo amekuwa akihusishwa mara kwa mara na kuhamia kwa Los Blancos hao tangu alipofanya vyema akiwa bado kijana mdogo kule AS Monaco.
Baada ya kuingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake mwaka 2021, Real Madrid ilitoa ofa ya wachezaji tisa kwa Paris Saint-Germain kwa ajili ya Mbappe mwishoni mwa dirisha la usajili la joto, lakini hilo lilikataliwa na miamba hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1.
Ulimwengu wa soka ulitarajia hatimaye Mbappe angejiunga na Real Madrid mwishoni mwa msimu huo kwa uhamisho wa bila malipo, lakini katika hali ya kushangaza, alitia saini mkataba mpya Parc des Princes Mei 2022.
Lakini PSG ilishindwa kutamba kama washindani wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati wa msimu wa 2022/23, na mapema kwenye kampeni Mbappe alikuwa tayari ameomba kuondoka kwa klabu hiyo. Huku PSG wakiwa tayari wamempoteza Lionel Messi kwa Inter Miami na Neymar pia huenda akaondoka kwani Newcastle Unite wanamtafuta.
Real Madrid wenyewe wamempoteza mshambuliaji Karim Benzema kwa mabingwa wa Saudi Pro League Al-Ittihad na wanawinda nyota mpya, huku Harry Kane wa Tottenham Hotspurs akiwa miongoni mwa walengwa wao wakuu.
Video kwenye mitandao ya kijamii ilimwonesha Perez akiulizwa kama timu yake itamsajili Mbappe. “Ndio, lakini sio mwaka huu,” alijibu.
Real Madrid tayari wameanza biashara yao ya uhamisho wa majira ya joto kwa kumsajili beki wa kushoto Fran Garcia kutoka Rayo Vallecano, huku Brahim Diaz akisaini mkataba mpya baada ya kumalizika kwa mkopo wake AC Milan.