Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewataka Wafanyabiashara wa Madini nchini, kuhakikisha wanarejesha nchini fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya madini nje ya nchi ili zisaidie kuimarisha uchumi wa nchi.
Biteko ameyabainisha hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na wafanyabiashara hao kutoka nchi nzima kilichohudhuriwa na Viongozi Waandamizi wa Wizara na Taasisi zake, Mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesema, Sekta ya Madini nchini imetawaliwa na uwekezaji wa mitaji kutoka nje ya nchi ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 5.1 cha Sera ya madini kinasisitiza ustawi wa masuala ya kiuchumi ikiwemo ustawi wa huduma za benki nchini ili kuleta manufaa kwa Serikali na sekta binafsi.
Aidha, Biteko ameongeza kuwa kutokana na kifungu hicho, Wizara ingependa kuona fedha za mauzo ya madini zinarejeshwa nchini kama Sheria inavyoelekeza kupitia mifumo ya kibenki na kwa kuzingatia sheria zote za nchi na kuongeza kwamba, hayo yote yanalenga kuboresha shughuli za madini nchini kutokana na umuhimu wa Sekta hiyo kiuchumi.