Wachezaji wa Simba SC wameripotiwa kuanza kuizoea hali ya hewa na Marrakech baada ya kutua jana Jumatano (Desemba 06) mchana tayari kwa mchezo wa keshokutwa Jumamosi dhidi ya Wydad Casablanca, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha akiwa hana presha kutokana na kutembea na faili la wapinzani wao anaowajua nje ndani tangu akiwa Algeria.
Simba SC itakuwa wageni wa Wydad katika mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi kuanzia saa 4:00 usiku kwenye Uwanja Marrakech, huku ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa na timu hiyo katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita kwa Penati baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1.
Tayari kila timu imecheza mechi mbili za Kundi B, huku Simba SC ikivuna pointi mbili baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ya lvory Coast na suluhu mbele ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, wakati wenyeji wao walipasuka michezo yote mbele ya wapinzani hao waliopata sare kwa Mnyama, hivyo kuifanya mechi iwe ngumu.
Hata hivyo, rekodi zinambeba Benchikha, Kocha mbobezi wa soka la Afrika hasa Kanda ya Kaskazini akiwa na msaidizi wake Farid Zemiti kwani wameshakutana na timu hiyo mara 10 na kushinda nne, kupoteza na mbili kuisha kwa sare kitu kinachomfanya asiwe na presha kubwa.
Benchikha kwa mara ya kwanza alikutana na Wydad Oktoba 14, 2013 akiwa kocha mkuu wa Difaa El Jadida ya Morocco katika Robo Fainali ya Kombe la FA la Morocco mechi iliyomalizika kwa sare ya mabao 1-1 lakini akamaliza mechi hiyo kibabe kwenye matuta chama lake likishinda 6-5 na kutinga Nusu Fainali.
Baada ya miaka kupita, msimu wa 2018/2019 alikutana tena na Wydad akiwa na Maolodia ambapo katika mchezo wa kwanza wa Februari 28, 2019 alipasuliwa 3-2 lakini zilipokutana tena Julai 29, 2020 zilitoka sare ya 1-1 kabla ya kuondoka Oktoba kujiunga na Difaa.
Desemba 9, 2020 alikutana tena na Wydad kwenye mechi ya Ligi na kupoteza kwa 1-0 lakini baada ya hapo alikutana nao tena Juni 9, 2021 kwenye mechi ya ligi na kupoteza tena 4-2, hata hivyo alilipa kichapo hicho kwenye mechi ya marudiano iliyopigwa Desemba 8, 2021 kwa kushinda 2-1 na msimu uliofuata akafungwa 2-1 Juni 22, kisha kufukuzwa na kukimbilia RS Berkane.
Akiwa na RS Berkane 2022, Benchikha alikutana na Wydad mara tatu akianza kwa kufungwa 2-0, kwenye mechi ya Ligi iliyopigwa Oktoba 2022, lakini akawaonyesha ubabe wake kwa kuwafunga mara mbili mfululizo akianza na 2-0, kwenye mechi ya kirafiki iliyopigwa Agosti 27 kisha kuwachapa tena 2-0, Septemba 10, 2022 kwenye Fainali ya CAF Super Cup na kubeba ndoo hiyo kubwa Afrika mbele yao.
Rekodi hizo ndizo zinaipa jeuri Simba SC kwenye mechi ijayo, pia matokeo ya hivi karibuni ya Wydad ikipoteza mechi nne mfululizo (kabla ya mchezo wa jana) yanaipa nguvu Simba SC ambayo imetoa sare mechi zake nne zilizopita.
Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni timu hizo zimeoneka na kuwa na mizani sawa kwani zilikutana mara mbili kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa na kila timu kupata matokeo ya 1-0, nyumbani kwake katika dakika 90 za kuhesabu ila Wydad ikasonga mbele kwa mikwaju ya Penati 4-3.
“Wydad imetoka kupoteza mechi mbili, haitakubali kufungwa, lakini nasi tunataka ushindi ili kujitengenezea nafasi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi.” amesema Benchikha.