Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya kuwa madarakani kwa rais aliye hai bila kuwajumuisha wafalme, anaapishwa tena ili kuongoza muhula wa sita, wa miaka saba.
Wanachama wa jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na serikali ya Marekani, wameibua wasiwasi juu ya uhalali wa ushindi wa kishindo wa chama cha rais huyo cha PDGE kilichojizolea asilimia 94.9 ya kura huku pia Wajumbe wa serikali ya nchi hiyo ya Afrika ya kati, wakikubali mashaka hayo.
Msemaji wa Serikali ya Equatorial Guinea, Atalia Ndong anasema, “Kitu pekee ambacho wananchi wanaweza kutarajia kutoka kwa rais mpya aliyechaguliwa tena ni kuendeleza maendeleo ya nchi katika sekta zote kwani inachokitarajia jaamii ya Guinea ni uendelevu wa sekta ya elimu, afya, uchumi na miundombinu.”
Aidha Ndong ameongeza kuwa, “Kila nchi ina kielelezo chake cha demokrasia, na hakuna mfumo unaosimamia demokrasia kwa ukamilifu na kwamba hata Equatorial Guinea ipo demokrasia ya rais, uchaguzi wa amani, na wanafurahi kuwa vyama vya upinzani vilishiriki na mmoja wa wagombea wakuu alitoa pongezi.
Akiwa madarakani tangu mwaka wa 1979, Obiang alichaguliwa tena katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta iliyopo Afrika ya Kati ambayo anaitawala kwa mkono wa chuma na katika kukabiliana na upinzani uliozidiwa maarifa huku akiwa na zaidi ya miaka 43 ya uongozini akishikilia rekodi ya kuwa mkuu wa nchi aliyekaa muda mrefu zaidi nje ya utawala wa kifalme.