Rapa wa kike, Remy Martin jana aliweka ukomo wa ushindi wa miaka saba mfululizo wa Nicki Minaj, baada ya kushinda tuzo ya rapa bora wa kike kwenye tuzo za BET 2017.
Remy Ma ambaye alitoka jela mwaka 2014, alitangazwa kuwa mshindi katika kipengele hicho kwa mwaka huu katika tuzo hizo zilizofanyika Los Angeles Marekani, tuzo ambayo ilizoeleka kuchukuliwa na hasimu wake Nicki Minaj tangu mwaka 2010.
Mara ya mwisho, Remy Ma alishinda tuzo hiyo mwaka 2005 na baadae kufungwa jela miaka mitatu baadae kwa kosa la kumpiga risasi rafiki yake wa zamani aliyemtuhumu kumuibia.
Akiwa jukwaani, Remy alimshukuru Mungu, familia yake, Fat Joe na mashabiki kwa kumuwezesha kufika hapo, huku akisisitiza kuwa unaweza kufanya kosa na ukarekebisha na kuendelea.
“Kwa yeyote anayefikiri hakuna kitu kama kupewa nafasi ya pili, niko hapa kuwaambia kuwa huo ni uongo. Unapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii tu,” alisema Remy Ma. “Unaweza kupata nafasi ya pili, unaweza kufanya makosa na kurejea tena,” alisisitiza.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Remy aliachia wimbo wa ‘diss’ ya moja kwa moja kwa Nicki Minaj, ambao ulipata sifa kila kona kutoka kwa wapenzi wa hip hop. Nicki hakutoa wimbo maalum wa kujibu diss hiyo lakini alimrushia makombora kwenye nyimbo nyingine rasmi alizofanya.