Kocha Mkuu mpya wa Singida Big Stars, Ricardo Ferreira ametamba kuchukua pointi tatu mbele ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans kutokana na kubaini mapungufu yao mengi kwenye mchezo huo.
Singida Big Stars itakuwa mgeni wa Young Africans Oktoba 27, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huo ukiwa ni mchezo wa pili kwa kocha huyo raia wa Brazil baada ya kuifunga Namungo FC katika mchezo wake wa kwanza Uwanja wa Majaliwa.
Kocha huyo amesema kwa namna alivyowaona wapinzani wao ana uhakika wa kutimiza ahadi yake ya kuchukua pointi tatu katika mchezo huo kwani amebaini makosa mengi ya Young Africans kwenye mchezo dhidi ya Azam FC uliopigwa juzi Jumatatu (Oktoba 23).
“Siwezi kusema hadharani lakini Young Africans ni timu ambayo inafungika tena kirahisi sana, nimewaonesha washambuliaji wangu madhaifu yao na nimewapa mbinu bora za kutumia ili kupata pointi tatu katika mchezo huo,” amesema Ferreira.
Kocha huyo amesema kilichowaponza Azam FC kushindwa kuifunga Young Africans ni wachezaji kushindwa kutimiza majukumu yao muhimu jambo ambalo wapinzani wao waliyatumia vyema makosa hayo kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa kwenye eneo la ushambuliaji.
Amesema anajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini uwezekano wa Singida kuibuka na ushindi katika mchezo huo ni mkubwa kutokana na mipango mkakati waliyokuwa nayo.
Ferreira ametua Singida kuchukua nafasi ya Mjerumani, Ernest Middendorp aliyesitisha mkataba wa kuifundisha timu hiyo kwa madai ya uongozi timu hiyo kumuingilia katika majukumu yake.