Kocha Mkuu mpya wa Singida Big Stars, Mbrazili Ricardo Heron Ferreira amesema yupo klabuni hapo kuhakikisha anaifanya timu yeke kuwa tishio katika Ligi Kuu na mashindano mengine wanayoshiriki.
Ferreira, ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja, amekuja na msaidizi wake Andrew Barbosa Deco kurithi mikoba ya Ernst Middendorp ambaye alitimka timu hiyo katika mazingira ya utata.
Ferreira amesema baada ya kufuatilia soka la Tanzania ameona kwa zaidi ya miaka 10 bingwa ni Simba SC na Young Africans tu, hivyo anakuja kuitengeneza Singida BS kuwa miongoni mwa timu zenye kuleta ushindani katika Ligi.
Ni kitu kizuri kupata nafasi ya kuinoa Singida na nipo hapa kwa ajili ya kutengeneza timu iwe bora, kwangu mimi natakiwa nifanye kitu cha tofauti.
“Nikiangalia mabingwa kwa miaka 10 nyuma naona majina ya Simba SC na Young Africans na nipo hapa kujaribu kufuta hilo kwa kuanzia kuitengeneza timu yenye ushindani wa hali ya juu, siwezi kuahidi kuchukua ubingwa bali kuleta ushindani wa kutosha.”
Ferreira amesema yote hayo hayawezi kutimia kimiujiza bali kwa kupata muda wa kukijenga kikosi chake vizuri hatua kwa hatua.
Kocha huyo ana uzoefu na soka la Afrika baada ya kuzinoa timu za Ismailia (Misri), Al Merrikh na Al Hilal zote za Sudan kwa nyakati tofauti.
Mtihani wa kwanza kwa kocha huyo ni Oktoba 21 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa.
Tayari kikosi cha Namungo FC jana Jumapili (Oktoba 15) kilianza safari ya kwenda Ruangwa, Lindi kwa ajili ya kuweka kambi ya mchezo huo.