Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Adenor Leonardo Bacchi (Tite), amemuita mshambuliaji wa klabu ya Everton, Richarlison de Andrade kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa mwanzoni mwa mwezi Septemba dhidi ya Marekani na El Salvador.
Richarlison mwenye umri wa miaka 21, ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa klabu ya Fluminense Pedro, Guilherme Abreu dos Santos ambaye alipata majeraha ya goti wakati wa mchezo wa ligi ya Brazil mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Cruzeiro walioibuka na ushidni wa mabao 2-1.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Watford, tayari ameshafunga mabao matatu katika michezo mitatu ya ligi ya England msimu huu, akiwa na Everton, lakini kwenye mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Bournemouth uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, aliadhibiwa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.
Brazil watacheza michezo hiyo ya kimataifa ya kirafiki kwa mara ya kwanza baada ya kutupwa nje ya fainali za kombe la dunia katika hatua ya robo fainli kwa kufungwa na Ubelgiji, mwezi Julai mwaka huu.
Brazil wataanza kucheza dhidi ya Marekani mjini New Jersey Septemba 7, na siku nne baadae watapambana na El Salvador mjini Maryland (Marekani).