Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameweka wazi namna ambavyo aliitwa na kuhojiwa na Ofisi ya Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini baada ya jina lake kujumuishwa katika orodha ya watuhumiwa.
Akizungumza jana na Erick Martin kwenye Habari Extra ya 100.5 Times Fm, Ridhiwani ambaye ni mtoto wa rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete alisema kuwa alihojiwa kwa muda na ofisi hiyo ambayo hata hivyo ilimuweka wazi kuwa baada ya uchunguzi wake haikumkuta na hatia.
“Katika mahojiano yetu, kikubwa zaidi waliniambia wao wamechunguza, kwa maana kwamba wamefuatilia mienendo yangu… na kwamba wao hawakukuta kuna jambo lolote ambalo linahusu mimi kujihusisha na dawa za kulevya,” Ridhiwani alisema.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Chalinze alisema ofisi hiyo ilimuweka wazi kuwa uchunguzi uliofanyika ulibaini yeye hukaa katika maeneo ambayo huzungukwa na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, lakini hawakupata ushahidi wowote unaoonesha kuwa anashirikiana nao kwa namna moja ama nyingine.
“Isipokuwa Kamishna alichoniambia, ambacho mimi niliambiwa kama ni angalizo, ni kwamba wapo baadhi ya watu katika maeneo ambayo mimi hupendaga kukaa ambao wao katika namna moja ama nyingine wanajihusisha na dawa za kulevya. Lakini walichoniambia ni kwamba hawajapata ushahidi kama ninashirikiana nao watu hao,” alisema.
Ridhiwani alieleza kuwa Ofisi ya Kamishna ilimpa angalizo kuwa aepuke kukaa katika maeneo ambayo watu hao huwepo kwani wanaweza kumtumia kama ngao yao katika kuendesha biashara yao.
Mwanasiasa huyo amekuwa akitajwa hasa kwenye mitandao ya kijamii akihusishwa na tuhuma za dawa za kulevya. Kwa mujibu wake, Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga alimuita baada ya kutajwa katika orodha iliyowasilishwa kwa kamishna huyo na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Makonda aliuwasha zaidi moto wa kupambana na biashara ya dawa za kulevya baada ya kutaja hadharani majina ya watuhumiwa wa dawa hizo ambapo katika orodha ya awali, aliwataja Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga ambaye pia ni mmiliki wa makampuni ya Quality Group Tanzania, Yusufu Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Wengine waliotajwa katika orodha hiyo ya Makonda ni wasanii mbalimbali akiwemo Vanessa Mdee na Wema Sepetu ambao katika nyakati tofauti walisota katika selo za polisi jijini Dar es Salaam kwa siku kadhaa wakishikiliwa kwa mahojiano.