Mbunge wa jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete amesema kuwa mkakati wa kuhakikisha maendeleo yanawafikia watu wa hali ya chini ndiyo msingi utakaowafanya wananchi waendelee kuipenda na kuichagua (CCM).
Ameyasema hayo jimboni humo alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika zahanati ya kitongoji Cha Chahua .
Amesema kuwa furaha yake juu ya mafanikio ambayo halmashauri ya Chalinze iliyopata ambayo yanatokana na msimamo ambao CCM inasimamia inapofika katika utekelezaji wa ilani yake .
“Katika halmashauri ya Chalinze tumejenga zaidi ya zahanati 86 katika vitongoji na vijiji, vituo vya afya zaidi ya 13 na sasa tunakamilisha hospitali ya wilaya ambayo sh. milioni 500 zinatarajiwa kuletwa kumalizia ujenzi pamoja na kununua vifaa tiba,” amesema Kikwete.
Aidha, amewataka wananchi jimboni humo kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ambazo Rais Dkt. Magufuli anafanya kwa kushirikiana nayeye, diwani na mwenyekiti wa kitongoji hicho.
Akizungumzia sula la elimu, amesema kuwa wanapambana kupunguza wingi wa wanafunzi shule ya sekondari ya Chalinze kwa kumalizia shule ya sekondari ya Pera na mkakati mwingine wa kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari ya Chahua.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa kitongoji hicho, Sadallah Maisha amemshukuru mbunge kwa kuwapatia nondo 80 na sh.milioni 2.5.