Vita dhidi ya dawa za kulevya ni kubwa na inapaswa kupigwa na kila mmoja ili kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wana athirika kutokana na tatizo hilo.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete mara baada ya kuhojiwa na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini kama anahusika na biashara hiyo haramu.
Amesema kuwa jamii inapaswa kusimama kwa kauli moja ili kuliokoa Taifa na nguvu kazi inayopotea ili liwe na vijana wanaojitambua na kutimiza wajibu wao.
“Naunga mkono vita hii ya dawa za kulevya nchini kwani itasaidia kurudisha nguvu kazi inayopotea kutokana na matumizi ya dawa hizo za kulevya kwa mzazi ambaye mtoto wake ameathirika na matumizi ya dawa hizo anajua uchungu wake na hasara zake,”amesema Ridhiwani.
Vile vile akizungumzia suala la marafiki zake kuhusishwa na biashara hiyo haramu amesema kuwa sio marafiki zake bali ni watu anaokutana nao katika maeneo mbalimbali anayotembelea.
Hata hivyo, Ridhiwani amesema kuwa mchakato huo wa kupambana na dawa za kulevya nchini umekuwa ukiwachanganya wananchi kwani haieleweki ni nani anayehusika na kushugulikia suala hilo la kuhoji.