Mwimbaji Rihanna ameisababishia kampuni ya Snap hasara ya takribani dola milioni 800 ($800 m) kutokana na ujumbe wake wa kulaani tangazo lililoonekana kwenye mtandao huo linalowavaa yeye na Chris Brown.
Maneno ya Rihanna dhidi ya Snap yalisababisha kushuka kwa mauzo yake katika soko la mauzo kwa asilimia 4.
Snap waliruhusu tangazo la mchezo (game) ambalo lilikuwa linawataka watumiaji kuchagua kimoja kati ya ‘kumpiga kofi Rihanna’ au ‘kumpiga ngumi Chris Brown’.
Chris aliwahi kupatikana na hatia na kuadhibiwa kwa kosa la kumshambulia kwa ngumi Rihanna mwaka 2009, wakati wawili hao walipokuwa wapenzi.
Tamko la Rihanna aliloweka Instagram, lilieleza hivi, kwa tafsiri isiyo rasmi:
“Sasa SNAPCHAT mnafahamu tayari kuwa mimi sio shabiki wa app yenu! Lakini ninajaribu kufikiria hii ilikuwa na maana gani! Ningependa kuuita ujinga, lakini naamini nyie sio wajinga kiasi hiki. Mmetumia pesa kutengeneza kitu ambacho kwa makusudi kitaleta aibu kwa muathirika wa unyanyasaji katika mahusiano na mmefanya iwe utani. Aibu yenu..!”
Hata hivyo, Snap wameeleza kuwa hawahusiki na tangazo hilo na kwamba liliwekwa na mteja wao na kwamba wanafanya uchunguzi kubaini lilifikaje kwenye app hiyo.
Snap pia wamemuomba radhi Rihanna ikiwa ni siku kadhaa tangu Kylie Jenner ailalamikie kwa kubadili mpangilio wake (design) ambao alidai sio rafiki kwa watumiaji. Malalamiko ya Kylie yalisababisha hasara ya dola za kimarekani 1.3 ($1.3b).